Jumamosi , 25th Jun , 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Prof. Joyce Ndalichako amefafanua kuwa kikokotoo kipya kinachotarajiwa kuanza tarehe 1 Julai mwaka huu, 2022

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Prof. Joyce Ndalichako akifafanua kuhusu Kikokotoo wakati akichangia mjadala makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2022/2023 Jijini Dodoma.

Amesema faida yake kubwa ni kuweka Uwiano na Usawa wa Mafao baina ya Wastaafu, ambapo watumishi wote wa sekta Binafsi na Umma watalipwa mafao ya mkupuo wa asilimia 33.

“Naomba nieleze Athari zilizokuwa zinajitokeza kwa kikokototoo cha zamani cha mkupuo wa asilimia 50, Mfano halisi ni Kuna mchangiaji katika mfuko ambaye amechangia kwa miezi 467 na michango yake kwa muda wa utumishi wake wote ni shilingi mil. 36, kanuni ya zamani alikuwa analipwa sh. milioni 129, yaani kachangia shilingi milioni 36 lakini anapata mafao ya mkupuo shilingi milioni 129. 

Ndalichako ameeleza “Wafanyakazi wengine ambao wamechangia shilingi milioni 86 na kufanya kazi kwa miezi 350 kwa kutumia mkupuo wa asilimia 25, anapata mafao ya mkupuo ya shilingi milioni 54. Huyu amechangia milioni 36 analipwa milioni 129, huyu amechangia milioni 86 analipwa milioni 54”

Akiongea wakati wa akichangia mjadala makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya serikali kwa mwaka 2022/2023.Mhe. Ndalichako ameeleza kuwa kikokotoo kipya kinaweka wafanyakazi wote wa Tanzania wa sekta ya binafsi na Umma, ambao wanasimamiwa na sheria za kazi na ajira zinazofanana kutumia viwango sawa vya ukokotozi wa mafao.

“Kikokotoo kipya kitaondoa utofauti kwa wastaafu ambapo baadhi walikuwa wanalipwa mkupuo wa asilimia 25 wakati wengine walikuwa wanalipwa mkupuo wa asilimia 50. Kikokotoo hiki kinasaidia kwa sasa mifuko ya pensheni inazungumza lugha moja.”

Ndalichako amefafanua kuwa serikali ni sikivu, kutokana na malalamiko ya watumishi na wadau kuhusu Kanuni za mwaka 2018 ambapo watumishi wote walikuwa wanalipwa mafao ya mkupuo kwa asilimia 25. Serikali ili sitisha kanuni hizo na kuagiza kamati maalum iliyowahusisha wadau wote ambao ni serikali, Waajiri na Waajiriwa. Lengo ilikuwa kuchambua hali ya uhimilivu na uendelevu wa mifuko. Aidha, ameongeza kuwa makubaliano yaliyofikiwa ndiyo yatakayo fanyika kuanzia Julai 1 mwaka huu.

Amefafanua kuwa kikokotoo kipya kitawasaidia watumishi kwa kuwa aliyechangia milioni 86 na mafao yake ya mkupuo yatapanda kuwa shilingi milioni 71 na ataendelea kulipwa pensheni ya kila mwezi shilingi mil. 1,840,000 mpaka Mwenyezi Mungu atakapo mwita.