Jumanne , 17th Mei , 2022

Polisi nchini Nigeria inawashikilia watu 4 kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya mhandisi wa sauti za muziki ambaye aliuawa na kundi kubwa la watu nchini humo.

Polisi wameongeza kuwa wanaendelea kuwasaka watu wengine kuhusiana na mauaji hayo.  

Mauaji ya David Sunday Imoh mwenye umri wa miaka 38 yameleta mdahalo mkubwa kwenye mitandao ya kijamii nchini Nigeria huku kukiwa na hashtag isemayo  #JusticeForDave  ikitapakaa kwenye mitandao ya kijamii.

Hakuna sababu zilizobainishwa juu ya mauaji ya kijana huyo ambaye alipigwa kama mwizi na kisha kuchomwa moto.  

Lakini kumekuwa na madai mitandaoni kwamba , yalitokea majibizano baina na David  na mwendesha bodaboda juu ya malipo ya safari baada ya kufikishwa kwenye club ambapo ndio  kazini kwake.

 
Mauaji haya yanatokea katika kipindi ambacho Wanaigeria wanaendeleza taharuki juu ya mauaji ya mwanafunzi wa kike  huko kaskazini mwa jiji la  Sokoto ambaye aliuawa kwa sababu ya kuikashifu imani ya kiislamu.