Jumanne , 6th Dec , 2022

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja, amesema serikali itaunda kamati ya kuangalia migogoro ya mipaka na vijiji vinavyozunguka msitu wa Hifadhi ya Bonde la  Wembere uliopo katika Halmashauri ya wilaya ya Iramba mkoani Singida.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja, akizungumza na wananchi wanaozunguka Hifadhi ya Bonde la Wembere

Ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi kuhusu mgogoro wa mipaka kwenye eneo la ardhi oevu katika Kijiji cha Msai na Ujungu mkoani Singida.

Amesema kamati hiyo itaishauri serikali endapo kuna umuhimu wa kurekebisha mipaka na kama eneo hilo litafaa kwa ajili ya shughuli za kibinadamu au la.

"Kuanzia leo tunaunda kamati ambayo itajumuisha wataalam kutoka ngazi ya Wizara, mkoa na wilaya na zoezi hilo litaanza mara moja na itapitia mipaka kwa kushirikiana na wananchi ili kuainisha mipaka halisi kwa kuzingatia ramani iliyopo ili kumaliza mgogoro huo," amesema Naibu Waziri Masanja.

Naibu Waziri huyo pia amewataka wananchi hao kuzingatia sheria za kutovamia maeneo ya hifadhi na kuwa walinzi wa eneo hilo mara tathmini itakapokamilika. 

Kuhusu changamoto ya wafugaji wanaopitisha ng'ombe katikati ya hifadhi kwa ajili ya kupeleka mifugo yao kunywa maji amesema, serikali itaangalia namna iliyobora ya kutatua changamoto hiyo ili wananchi wasiingiliane na masuala ya uhifadhi.

Naye, Mbunge wa Iramba Magharibi ambaye pia ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka viongozi wa Kata na vijiji kushirikiana na kamati iliyoundwa wakati wa kupitia upya usahihi wa bikoni zilizowekwa.