Alhamisi , 6th Mei , 2021

Wananchi wa Kijiji cha Mawenzusi, Sumbawanga mkoni Rukwa, wamelalamikia utapeli unaofanywa na waganga wanaojiita lambalamba wanaopita majumbani na kuwaaminisha kuwa wamewekewa vitu vya kishirikina na mahasidi wao na wakiingia ndani hufukia vitu vyao na kisha kuvitoa na kutaka walipwe.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Mwenzusi, Sumbawanga

Wananchi hao wametoa kero hiyo mbele ya mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfani Haule, mara baada ya kuwatembelea katika kijiji hicho alipokuwa akikagua miradi ya maendeleo huku mwenyekiti wa kijiji hicho akikiri kushindwa kudhibiti utapeli huo.

"Nimekaa kupinga vitendo hivyo mpaka nimekaliwa vikao na vijana kiasi kwamba hata kutembea kwangu ni kwa wasiwasi", ameeleza mmoja wa wananchi hao

"Suala la lambalamba ni tatizo sana hapa kijijini ninaomba msaada wa kufa na kupona, niokolewe kwa sababu itafika wakati madhara yatatokea na itaonekana kwamba mimi Mwenyekiti ninahusika", ameeleza Mwenyekiti wa Kijiji hicho
 
Naye mwenyekiti wa waganga wa tiba asili mkoani Rukwa, Michael Jackson, amekemea vikali suala hilo huku akisema kuwa suala hilo halitambuliki kwa mujibu wa sheria zao na hivyo kinachofanywa ni wizi na utapeli kwani hawana vibali.

Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfani Haule, amesema kuwa watu hao wamepita kila vijiji vya wilaya hiyo na baadhi yao wamekwishakamatwa hivyo serikali itawachukulia hatua na mkondo wa sheria lazima ufuatwe.