Jumamosi , 25th Jun , 2022

Bodi ya Utalii Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Kusini imetumia maonesho ya Seoul International Tourism Expo (KOTFA 2022), kuonesha Makala ya The Royal Tour Tanzania kwa Mawakala wa utalii pamoja na Waandishi wa habari za utalii katika soko ya utalii nchi hiyo.

Maonesho yameanza tarehe 23 – 26, 2022.

“Nashukuru leo tumefanikiwa kukutana na wadau wa utalii wa hapa Korea Kusini, huu ni mwanzo mzuri na tutaendelea na utaratibu huu ili wadau waweze kuvijua zaidi vivutio vya utalii vya Tanzania. Baada ya kuona filamu ya The Royal Tour, TANZANIA, wamependa kujua fursa za uwekezaji zilizopo Tanzani, jambo ambalo linaleta matumaini kwa Mawakala wa utalii wa nchi hii kuanza kuuza utalii wa Tanzania.

Hayo yamesemwa na  Balozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Balozi Togolani Edriss Mavura wakati wa mkutano  uliofanyika Juni 24, 2022 katika hotel ya Intercontinental Seoul Pama iliyopo  katika mji wa Seoul.

Naye Afisa Habari na Uhusiano wa Bodi ya Utalii Tanzania, Bi.  Augustina Makoye ametumia mkutano huo kuwakaribisha wawekezaji kutoka Korea Kusini kwani Tanzania bado ina fursa za uwekezaji katika sekta ya utalii hasa kwa upande wa  Malazi, Migahawa na huduma nyingine, ili iwe chachu ya kuwavutia watalii wengi kutoka katika soko la utalii la Korea.

Aidha, wakati anatoa neno la shukrani, Bi. Augustina ametumia muda huo kuwaalika Mawakala wa utalii wa Korea Kusini kushiriki Onesho la Utalii la Swahili International Tourism Expo (SITE) linaloandaliwa na Bodi ya Utalii Tanzania. Onesho hilo limepangwa kufanyika wiki ya mwisho ya mwezi Oktoba 2022 jijini Dar es Salaam, na ameahidi kuwatumia mwaliko punde maandalizi ya onesho hilo yatakapo zinduliwa rasmi.