Jumanne , 12th Oct , 2021

Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima, anatarajia kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika Kongamano la tatu la Kimataifa la Wanawake litakalofanyika nchini Urusi kwa siku tatu kuanzia Oktoba 13 hadi 15, 2021. 

Waziri wa Afya, Dkt. Dorothy Gwajima,

Akiwa nchini Urusi, Dkt. Gwajima atashiriki katika ufunguzi wa kongamano hilo ambapo ataonesha namna Tanzania ilivyofanikiwa katika kuwa na usawa wa kijinsia, kuwainua wanawake kiuchumi na kutambua mchango wao katika maendeleo ya Taifa.

Dkt. Gwajima anashiriki katika kongamano hilo ikiwa ni mwelekeo na azma ya serikali ya awamu ya sita katika kuhakikisha uwepo wa usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa wanawake katika nyanja mbalimbali.

Aidha, lengo kuu la kongamano hilo ni kutambua mchango wa wanawake katika maendeleo ya Dunia, kuonesha mchango wa wanawake katika maendeleo na kuhakikisha kunakuwa na usawa wa kijinsia.