Ijumaa , 24th Jun , 2022

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Dkt Dorothy Gwajima, ameripoti kwa viongozi wa mtaa wake anaoishi wa Ilazo Mbuyuni kwa lengo la kukutana na kujadiliana na viongozi hao wa Mtaa wa Ilazo Mbuyuni, Kata ya Ipagala jijini Dodoma ili kuweka mbinu za kukabiliana na ukatili wa kijinsia kwenye jamii.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maaalum, Dkt Dorothy Gwajima

Akizungumza na uongozi wa Kata hiyo Dkt. Gwajima, amesema mbinu za kutokomeza ukatili lazima zitokane na wanajamii wenyewe kwa sababu wanaofanya ukatili wanatoka miongoni mwao.

"Sisi wanajamii ya Ipagala lazima tuungane na jamii ya Watanzania wote kuitikia wito wa serikali katika kupambana na ukatili na ikiwezekana tuwe wa kupigiwa mfano na jamii zingine," amesema  Dkt. Gwajima.

 Kuhusiana na takwimu za ukatili, Waziri Dkt Gwajima alisema, matukio yaliyoripotiwa kwa mwaka 2021 yalikuwa zaidi ya 11000 kwa watoto, huku matukio ya ubakaji yakiwa zaidi ya 5000.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilazo Mbuyuni Lucas Mwasongwe, alimpongeza Waziri kwa kushuka na kujadili suala hilo katika ngazi ya chini na kuwaomba viongozi kuiga mfano huo.

"Mtoto akitoka shule kaa naye, mdadisi mfanye kuwa rafiki, kataeni vitendo vya ukatili vimekithiri kama alivyosema Mhe. Waziri" alisema Mwasongwe.