Alhamisi , 18th Mei , 2017

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Christina Mdeme amewaagiza wamiliki wa shule na mabasi yanayobeba wanafunzi kusimamia nidhamu ya madereva ili kuepuka madhara yaonayoweza kutokea kutokana na uzembe.

Bi Mdeme ametoa kauli hiyo wakati akiongea na wamiliki wa shule na mabasi ya wanafunzi mkoani humo katika kikao cha pamoja kwa ajili ya suala la ukaguzi na usalama wa magari ya wanafunzi mjini Dodoma.

Mkuu huyo wa Wilaya amesema kuwa wakati mwingine ajali zinatokea si kwa ubovu wa magari hayo bali ni tabia za madereva ambazo zinapelekea kutokea kwa ajali hivyo bila kusimamiwa kwa nidhamu yao bado matukio kama hayo yataendelea kutokea.

Katika hatua nyingine Bi. Mdeme amepiga marufuku kuwajaza wanafunzi katika gari moja kupita idadi yao huku akiongeza marufuku ya kusafirisha wanafunzi hasa wa shule za awali na msingi kwa njia ya bodaboda.