Jumatatu , 17th Jul , 2017

Mbunge wa Singida Mashariki na Rais wa Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS), Tundu Lissu amesema Ukawa unatangaza vita na CUF ya Profesa Ibrahim Lipumba kama walivyo vitani na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Lissu ameyasema hayo leo wakati wa mazungumzo na waandishi wa habari katika makao makuu ya chama hicho yaliyopo Kinondoni, Jijini Dar es salaam.

“Profesa Lipumba ametusaliti kwa kuwa yeye ndiye aliyempitisha Lowassa kuwa mgombea wa urais kwa tiketi ya Ukawa. CUF ya Lipumba ilitusaliti kama Yuda Iskarioti alivyomsaliti Yesu Kristo,” amesema Lissu.

Mgogoro wa CHADEMA na CUF ya Lipumba ulianza baada ya kiongozi huyo kuandika barua ya kujiuzulu Uenyekiti wa chama hicho wakati wa uchaguzi mkuu mwaka 2015 na baadaye kutaka kurejea katika nafasi yake hali iliyosababisha mpasuko ndani ya Ukawa pamoja na CUF kwa ujumla.