Jumapili , 15th Mei , 2022

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia ongezeko la mishahara na kupandishwa kwa malipo ya mkupuo ya pensheni kwa wastaafu, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 -2025

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Shaka Hamdu Shaka.

Taarifa hiyo imetolewa leo Mei 15, 2022, na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho, Shaka Hamdu Shaka, na kusema uamuzi huo wa kupandisha mishahara, ikiwa ni pamoja na kima cha chini kwa watumishi wa umma kwa asilimia 23.3, ambao umefanyika kwa kuzingatia taratibu za mwenendo wa uchumi, pia ule wa kuelekeza kukamilishwa kwa taratibu za kisheria kuhakikisha malipo ya mkupuo ya wastaafu yanapandishwa kutoka asilimia 25 hadi asilimia 33. 

"Utekelezaji wake umedhihirisha jinsi Rais Samia Suluhu Hassan, alivyo kiongozi msikivu, anayejali wananchi wake, muungwana wa vitendo na zaidi yuko imara kuhakikisha serikali ya CCM anayoiongoza, inaendelea kuwa tumaini la watu kwa kugusa maisha yao kwa namna chanya,"imeeleza taarifa hiyo

Taarifa hiyo  ikatoa wito kwa wafanyakazi wa ndani kwamba waendelee kuiunga mkono serikali, kushikamana, kufanya kazi kwa bidii, uzalendo na weledi ili kuleta tija zaidi katika maendeleo ya nchi.