Jumapili , 9th Mei , 2021

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Pauline Gekul amezitaka Halmashauri zote nchini kusimamia michezo kuanzia ngazi za vijiji ili wananchi  waweze kuimarisha afya zao  na kukuza michezo kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa.

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe.Pauline Gekul

Mhe. Gekul ametoa maagizo hayo Mei 08, 2021 Jijijini Mbeya akiwa Mgeni Rasmi katika Mbio za Tulia Marathon  zinazodhaminiwa na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini ambaye pia ni  Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Tulia Ackson.

"Nafahamu kuna asilimia 40 inayotengwa na Halmashauri kwa ajili ya shughuli za maendeleo, natoa rai kwa viongozi wa Halmashauri kutenga fedha kidogo kwenye hiyo asilimia ambazo zitawezesha shughuli za michezo kwenye maeneo yenu kuanzia ngazi za chini kabisa kwenye vitongoji", amesisitiza Mhe. Gekul.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Mhe. Dkt. Tulia Ackson amesema lengo la mashindano hayo ni kuboresha Miondombinu ya Elimu na Afya kupitia Taasisi ya TuliaTrust Fund kwenye Jimbo hilo ambapo zinatarajiwa kufikia Watanzania wengi hapo baadae.

"Tulia Trust Fund ipo kwa ajili ya kusadia na kuwezesha wananchi kiuchumi,tangu mwaka 2018 taasisi hii imesadia wananchi kupitia miradi mbalimbali ikiwemo kuboresha madarasa, mabweni na upatikanaji wa maji na kazi inaendelea" amesema Mhe.Tulia.