Ijumaa , 16th Jul , 2021

Balozi wa Tanzania nchini Afrika ya Kusini Meja Jenerali (Mst) Gaudence Milanzi, amesema kuwa hadi sasa bado hajapokea taarifa rasmi kama kuna Mtanzania yeyote aliyeshiriki katika maandamano yanayoendelea nchini humo ama kuathiriwa biashara zake.

Polisi wakikabiliana na uporaji katika maduka nchini Afrika Kusini

Kauli hiyo ameitoa hii leo Julai 16, 2021, wakati akizungumza kwenye kipindi cha Supa Breakfast Menu Mpya cha East Africa Radio na kueleza kuwa wamekuwa wakijitahidi kuwasiliana na Jumuiya za Watanzania nchini humo, ili waweze kupata taarifa ya kile kinachoendelea katika maeneo yao.

"Mpaka sasa hivi hatujapata tarifa yoyote rasmi kama kuna Mtanzania kaharibiwa biashara ama kuhusika kwenye maandamano, lakini tunawasiliana na Jumuiya za Watanzania waendelee kutupa taarifa kila siku juu ya nini kinaendelea," amesema Balozi Milanzi.

Aidha, Balozi Milanzi ameoongeza kuwa, "Licha ya kwamba hatuna taarifa lakini tunachojua tu ni kwamba maeneo yote sasa hivi karibu wote wameathirika, basi kama siyo kwenye biashara zao lakini hali kwa ujumla, mfano kwa Zulu-Natal maisha yamekuwa magumu sababu maduka yamefungwa wala magari hayatembei".