Alhamisi , 24th Mei , 2018

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage amewataka wanafamilia, wafanyakazi na watanzania kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu ambapo Taifa limepoteza maofisa watatu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Waziri Mwijage amesema hayo leo Mei 24, 2018 katika ibada ya kuaga miili ya waliokuwa wafanyakazi watatu wa kituo cha uwekezaji waliofariki katika ajali ya gari eneo la Msoga na kuongeza kuwa anatambua wakati mgumu wanaopitia familia ya watumishi hao kwa kupoteza wapendwa wao kwasababu hata yeye alimpoteza mama yake akiwa na miaka sita.

“Hakuna zaidi ninaloweza kufanya, familia ni muhimili, uzoefu wangu mbaya hauwezi kuwa nafuu kwenu lakini hawa watoto wadogo wanaweza kufanana na mimi, nilimpoteza mama yangu nikiwa nina miaka sita lakini haya ni mapenzi ya Mungu” amesema Mwijage.

Waziri Mwijage ameongeza kuwa, Taifa limepoteza watu muhimu katika jitihada za kukuza sekta ya uwekezaji nchini na kuwataka wafanyakazi wengine wa kituo hicho kutohuzunika sana bali wawakumbuke wenzao kwa kufanyakazi kwa bidii.

Mei 21, 2018 katika eneo la Msoga mkoani Pwani watumishi watatu wa Kituo cha uwekezaji Tanzania (TIC) walifariki Dunia baada ya gari waliyopanda kugongana na lori walipokuwa wakisafiri kikazi kuelekea Dodoma, waliofariki ni Martin Laurence (39), Zakaria Nalinga (49) na Said Moshi.