Jumapili , 17th Jul , 2022

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetaja viwanja saba ambavyo vimekosa sifa za kutumika kwa michezo ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2022/2023.

Uwanja wa Sokoine (Mbeya)

Katika tathimini iliyofanywa na TFF wamebaini uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, Ilulu Lindi, Usharika (Kilimanjaro), Mabatini (Pwani), Sokoine (Mbeya), Jamhuri (Dodoma) na Nyankumbu Girls (Geita).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na idara ya habari ya mawasiliano ya Bodi ya Ligi imethibitisha kuwa kwa mujibu wa kanuni za ligi na sheria namba moja kati ya 17 za mpira wa miguu viwanja hivyo vimekosa sifa katika baadhi ya maeneo.

Walitaja maeneo hayo kuwa ni eneo la kuchezea kutokuwa tambalale na kukosa nyasi za kutosha, ubovu katika uzio wa kutenganyisha mashabiki na eneo la kuchezea, jukwaa kuu kubosa ubora ikiwemo ubovu wa paa.

Pia vyumba vya kuvalia nguo waamuzi na wachezaji vimekosa sifa za ukubwa stahiki pamoja na feni au AC kwaajili ya upatikanaji wa hewa ya kutosha, upatikanaji wa majisafi na ya kutosha muda wote, upatikanaji umeme na uwepo wa vyoo safi na vya kisasa.

Ilisema kukosekana kwa chumba cha mawasiliano, kukosekana kwa chumba cha madaktari kwaajili ya huduma ya kwanza, kukosekana kwa chumba kwaajili ya maofisa wa mchezo, kukosekana kwa mabenchi ya ufundi bora na yenye uwezo wa kuruhusu watu wasiopungua 17 kukaa, kukosekana kwa majukwaa kwaajili ya watazamaji na uwepo wa mabango au picha za matangazo zisizotambulika na TFF au TPLB.