Jumanne , 17th Jan , 2017

Mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania Bara, Yanga imezidi kuwafanya wapenzi wa Simba kuishi kwa wasiwasi baada ya leo kuchukua point 3 kwa Majimaji ya Songea, na kufikisha point 43, ikiwa ni point moja tu nyuma vinara wa ligi, Simba SC.

Yanga na Majimaji (Maktaba)

Katika mchezo wa leo, Yanga imetumia uzoefu na ukubwa wake katika ligi hiyo, ha kufanikiwa kupata bao pekee katika dakika ya 14 kupitia kwa Deus Kaseke aliyemalizia mpira uliopanguliwa na kipa wa Majimaji wakati akicheza kros ya Haruna Niyonzima kutoka winga ya kushoto.

Majimaji ambao wako chini ya udhamini mpya na kocha Kally Ongala, katika mchezo wa leo wameonesha mchezo wa ushindani huku wakimiliki mpira zaidi ya Yanga, lakini wamekosa mbinu ambazo zingeweza kuleta madhara kwenye lango la Yanga.

Hadi mwisho wa mchezo kutoka katika dimba la Majimaji Songea, Yanga bao 1, Majimaji 0.

Matokeo haya yanaiongezea Yanga mtaji wa kusaka kukaa kileleni kwani endapo Simba watashindwa kupata point 3 katika mcheo wa kesho,tofauti itakuwa ni point moja, ambayo itawafanya wawe na nafasi nzuri ya kuwashusha Simba kileleni.

Kwa upande wao Simba wanashuka dimbani kesho kukipiga na Mtibwa Sugar katika dimba la Jamhuri Morogoro.