Jumamosi , 22nd Apr , 2017

Mabingwa watetezi wa Ligi kuu ya Soka Tanzania Bara Young Africans wamefuzu na kuingia Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Tanzania Bara baada ya kuichapa Tanzania Prisons FC bao 3-0 mchezo uliopigwa katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam

Kikosi cha timu ya Yanga

Katika mtifuano huo, timu ya Yanga iliweza kujitengenezea mazingira mazuri ya kupata ushindi kwa kutumia akili nyingi na juhudi, mwishowe wakafanikiwa kujiandikia bao la kwanza kupitia mshambuliaji wake Amisi Tambwe kwa kuunganisha pasi ya kichwa mnamo dakika ya 15.

Vile vile ilipofikia dakika 40 timu ya Yanga iliweza kuwainua tena mashabiki wake kwa kupata bao la pili lililofungwa na Mzambia Obrey Chirwa baada ya kuunganishiwa pasi mujarabu ya kichwa kutoka kwa Haji Mwinyi na mpaka kipindi cha kwanza timu ya Prisons haikuweza kuona nyavu za mpinzani wake japokuwa walionesha jitihada zote.

Kwenye dakika 46 za kipindi cha pili cha mchezo, timu ya Yanga iliweza kuongeza bao jingine la tatu baada ya kufyatuliwa mkwaju mkali kutoka kwa mshambuliaji Saimon Msuva na kuifanya timu hiyo kuwa mbele zaidi kwa mabao 3 dhidi ya wapinzani wao Wajelajela.

Kutokana na ushindi huo, timu ya Yanga imeweza kuungana na timu nyingine tatu ambazo zilikuwa tayari zimeshafuzu hatua ya Nusu Fainali ambazo ni Mbao FC, Simba SC pamoja na Azam FC.

Kwa upande mwingine, siku ya kesho Jumapili ndiyo itakuwa siku ya mchakato wa droo ya kupanga ratiba za Nusu Fainali ya kujua nani atapangwa na nani.