Jumatatu , 17th Jul , 2017

Kamati ya Yanga imewateua Mohamed Nyenge, Tonny Mark na Majid Suleiman kuwa wajumbe wa kamati hiyo ili kujaza nafasi zilizokuwa wazi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na idara ya habari na mawasiliano ya klabu hiyo, uamuzi huo umefanywa katika kikao cha kamati hiyo kilichofanyika tarehe 15/07/2017 ikiwa ni kwa mujibu wa ibara ya 28(1)(d) ya katiba ya Yanga.

Taarifa hiyo imesema kuwa lengo la uteuzi huo ni kujaza nafasi mbili zilizokuwa wazi, na moja iliyoachwa na mjumbe ambaye alikuwa ni mwenyekiti wa kamati ya mashindano aliyekwenda nje ya nchi kwaajili ya masomo.

Wakati huo huo, makamu mwenyekiti wa klabu hiyo Clement Sanga mwishoni mwa wiki alikutana na wachezaji wa zamani waliopitia klabu hiyo na kuazimia kushirikiana ikiwa ni pamoja na kuwaweka wachezaji hao karibu na klabu.

Katika kufanikisha ushirikiano huo, Sanga na wachezaji hao wamekubaliana kuunda safu ya uongozi wao itakayorahisisha mawasiliano baina yao na uongozi wa klabu, kuweka kumbukumbu kwaajili ya historia ya klabu na vizazi vijavyo kupitia wao, pamoja na kusaidiana katika suala zima la ugunduzi wa vipaji vya wachezaji kwa manufaa ya klabu.