Jumatatu , 28th Sep , 2020

Uongozi wa Klabu ya Yanga kupitia kurasa zao za mitandao ya kijamii na tovuti yao imechapisha taarifa za kusikitishwa na kitendo kisicho cha kiungwana kilichofanywa na baadhi ya mashabiki wake cha kuwapiga na kuwafanyia vurugu mashabiki wa Simba siku ya jana tarehe 27.9.2020 kwenye Uwanja

Mashabiki wa Yanga wakitamba katika Uwanja wa Mkapa.

Taarifa ya Kaimu Katibu Mkuu, Wakili Simon Patrick imesema pamoja na kusikitishwa na kitendo hicho, uongozi wa Yanga pia unalaani vikali tabia hiyo inayojengeka ya uvunjifu wa amani katika soka na kuviomba vyombo vya Ulinzi na Usalama kuchunguza na hatimaye kuwachukulia hatua za kisheria wale wote watakaobainika kuhusika na vitendo hivyo.

"Yanga tunaamini Mpira ni furaha na sio uadui na tunawakumbusha mashabiki wetu kwamba upinzani wetu na Simba unatokana na UTANI WA JADI na siyo uhasama," imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha uongozi wa Yanga umewashukuru Wanachana, Wapenzi na Mashabiki wa Morogoro na maeneo mengine waliojitokeza kuiunga mkono timu yao na kufanikisha kupata ushindi katika mchezo huo.

Jana katika mchezo dhidi ya Mtibwa Sugar baadhi ya Mashabiki waliwafanyia fujo baadhi ya mashabiki wa Simba waliokuwa wakitazama mpira na kuishangilia Mtibwa Sugar Kama ambavyo imezoeleka katika utani wa jadi baina ya Yanga na Simba.