Jumatano , 18th Jan , 2017

Vinara wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara, Simba SC leo watajaribu kusogea mbali na wapinzani wao katika mbio za ubingwa watakapokuwa wageni wa Mtibwa Sugar katika Uwanja wa Jamhuri, Morogoro.

Mechi ya Simba Vs Mtibwa, mzunguko wa kwanza

 

Msemaji wa Mtibwa Sugar Thobias Kifaru amesema, Simba wasitarajie jambo la ushindi kuwa jepesi kutokana na hali halisi ya kikosi cha Mtibwa Sugar kwa sasa na dhamira yao ya kutotaka kupoteza mechi.

Kifaru pia amesema Simba ni kama watoto wa Mtibwa kwa kuwa wachezaji wake wengi wametoka Mtibwa, hivyo wanawajua vizuri na watatumia udhaifu wa wachezaji hao kuwaadhibu.

"Simba tumewalea sisi, vijana wetu hao wako hapo, akina Shiza Kichuya, Mohamed Ibrahim, Mzamiru wote hao wamekuliwa kwenye mashamba ya miwa, tunajua udhazaifu wao" Amesema Kifaru.

Kocha Mkuu, Mcameroon Joseph Marius Omog amesema, dhamira yao ni kucheza kila mechi kama fainali kuhakikisha wanashinda.

Mara baada ya Yanga kushinda 1-0 dhidi ya wenyeji Majimaji mjini Songea mkoani Ruvuma jana, iliikaribia Simba kwa tofauti ya moja kutoka nne hivyo Simba leo watakuwa na jukumu la kupigania ushindi ili kurudisha 'gap' la pointi nne na kuendelea kuongoza vizuri mbio za ubingwa.