Jumatatu , 13th Feb , 2017

Katika harakati za kuendelea kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, Shirikisho la Soka nchini TFF, linatarajia kuwapeleka vijana walio katika timu ya taifa ya Serengeti Boys katika kituo cha kusaidia waathirika wa dawa za kulevya cha Bagamoyo.

KIkosi cha Serengeti Boys

Shirikisho limesema lengo ni kuweza kupata mafunzo ambayo yatawasaidia kujikinga na matumizi hayo.

Afisa habari wa Shirikisho la Soka nchini TFF Alfred Lucas amesema, ziara ya vijana hao wa timu ya Serengeti Boys itakayofanyika Machi 04 mwaka huu itawasaidia kuweza kupata mafunzo ambayo yatawajenga na pia kuweza kujikinga kuingia katika matumizi ya dawa za kulevya ambazo zinaendelea kupoteza nguvu kazi ya Taifa.

"Tunaungana na serikali kupinga matumizi ya dawa za kulevya kwani zinazidi kuangamiza vijana ambao ndiyo nguvu kazi ya taifa, hawa vijana wapo katika umri ambao wanakumbwa na vishawishi vingi na tunaamini mafunzo watakayoyapata watayazingatia kwa faida yao binafsi," amesema Alfred.

Amesema, lengo la ziara hiyo pia ni sehemu ya kutekeleza moja ya kanuni za ligi ambazo zinapinga matumizi ya dawa za kulevya pamoja na ubaguzi katika soka.