Jumatano , 31st Jan , 2018

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia  na Ufundi, William Ole Nasha, amefafanua kuwa Baraza la Mitihani hufanya mchakato wa kutoa vyeti mbadala au uthibitisho kwa mtu aliyepoteza vyeti orijino ndani ya siku 30.

Ole Nasha ameeleza hayo bungeni leo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mafinga Mjini, Cosato Chumi (CCM) lililouliza ni utaratibu gani unaotumika pale mtu anapopoteza cheti ili aweze kupata cheti kingine na kama anapata cheti halisi au nakala.

Naibu Waziri huyo amesema kuwa mhitimu aliyepoteza cheti hupatiwa cheti mbadala/uthibitisho wa matokeo baada ya kufuata taratibu kadhaa ikiwemo kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi kuhusu upotevu wa cheti na kupata hati ya upotevu. Pia atatakiwa kutangaza gazetini kuhusu upotevu huo.

‘’Mhitimu hutakiwa kujaza fomu ya Baraza la Mitihani baada ya kufuata taratibu zote kisha Baraza hufanya uchunguzi wa uhalali wa umiliki wa cheti husika na kutoa huduma stahiki ndani ya siku 30'', amesema Ole Nasha.

Aidha Ole Nasha amesema kuwa wahitimu waliofanya mtihani kuanzia mwaka 2008 hupatiwa vyeti mbadala huku wale waliofanya mtihani kabla ya Mwaka 2008 hupatiwa uthibitisho wa matokeo ambao hutumwa sehemu unayohitajika.