Jumatatu , 30th Nov , 2020

Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dkt. Benson Bana amesema ushindi wa Simba SC dhidi ya Plateau United ni ushindi wa taifa kwa ujumla na mwaka 2020 kwa Tanzania ni mwaka wa ushindi.

Balozi wa Tanzania nchini Nigeria Benson Bana ( wa kwanza kushoto) akiwa na viongozi wa Simba SC.

Balozi Bana ameeleza hayo jana usiku baada ya mchezo wa kwanza hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika, ambapo Simba SC ilishinda 0-1 dhidi ya Plateau United.

"Ushindi wa leo ni ushindi wa Watanzania. Vijana wamefanya kile kilichotarajiwa na Watanzania, na sasa tujipange kwaajili ya mchezo wa marudiano na mwaka 2020 kwa Tanzania ni mwaka wa ushindi."- Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dkt. Benson Bana.

Kwa upande wake kocha wa Simba Sven Vandenbroeck amesema, "Ulikuwa mchezo mgumu, wana nguvu na walijaribu kiufundi kutafuta goli lakini nawapongeza wachezaji wangu sababu dakika zote 90 walikuwa wanakimbia kuzuia. Nafikiri tunatakiwa kuwa na furaha sana na ushindi. Matokeo mazuri lakini bado hatujamaliza sababu wiki ijayo tuna dakika 90 zingine".

Benchi la ufundi la Simba SC chini ya kocha mkuu Sven Vandenbroeck (katikati).

Simba SC imeanza safari ya kurejea Tanzania alfajiri ya leo Novemba 30, 2020 na inatarajiwa kutua kesho Jumanne Saa 10:00 jioni, kwenye uwanja wa ndege wa Kilimanjaro.

Mchezo wa marudiano utapigwa Desemba 5, 2020 kwenye uwanja wa Mkapa jijini Dar es salaam, ambapo Simba SC inahitaji sare ya aina yoyote ili kusonga mbele.