Jumatano , 21st Jun , 2017

Shirikisho la Soka nchini TFF, Kamati ya Uchaguzi imeanza kupitia fomu za wagombea hao kwa ajili ya kuanza zoezi la mchujo na kwa wale ambao hawana vigezo watajulishwa kabla ya mchakato kuendelea.

Rais wa TFF, Jamal Malinzi

Afisa habari wa TFF Alfredy Lucas amesema mara baada ya zoezi hilo kukamilika wagombea ambao watawekwa kando katika uchaguzi huo watajulishwa kabla ya kuendelea na mchakato unaofuata ndani ya Kamati ya uchaguzi.

“Mara baada ya wanafamilia 74 kumaliza zoezi la kuchukua na kurudisha fomu hapo jana ambapo 10 wanawania nafasi ya Rais, sita nafasi ya makamu na 58 wanawania Ujumbe wa kamati ya utendaji. Kinachoendelea kwa sasa ni kwa kamati ya uchaguzi ya TFF kuanza kupitia fomu moja baada ya nyingine na lengo likiwa ni kufanya mchujo wa awali kwa vile vitu vinavyohitajika kwenye fomu kama havijatimia, ” amesema Alfredy Lucas.

“Maana yake ni kwamba mgombea huyo anawekwa kando lakini wakati huo kwa mujibu wa kanuni ya 11 kipengele cha kwanza ya uchaguzi wa TFF watajulishwa kwa barua rasmi kwamba sababu hasa za kuwekwa kando ni nini na kama ataweza kukata rufaa ni sawa, lakini walishaelekezwa nini cha kufanya na kila mmoja ameweza kutimiza kile alichotakiwa kukifanya mpaka jana lakini kwa sasa tuiache kamati kwa siku hizi tatu kwa maana leo, kesho na kesho kutwa na baadae tutatoa taarifa au kubandikwa kwenye mbao za matangazo kile ambacho kimeonekana kwenye mchujo huu wa awali wa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa TFF, ” amesema Alfredy Lucas.

Nafasi ya Urais inawaniwa na Jamal Malinzi, Imani Madega, Wallace Karia, Fredrick Masolwa, Athumani Nyamlani, Fredrick Mwakalebela, John Kijumbe, Shija Richard, Ally Mayay na Emmanuel Kimbe.