Jumatatu , 14th Aug , 2017

Mlinzi kutoka ya timu ya TMT, Raphael Msofe amesema kilichosababisha wao kufungwa katika mechi ya jana dhidi ya Mchenga BBall Stars ni kutokana na baadhi ya wachezaji waliwahi kucheza rafu nyingi na kupelekea kufungwa.

TMT ilipachikwa pointi 101-71 dhidi ya wapinzani wao Mchenga BBall Stars katika mechi ya ufunguzi wa fainali ya Sprite BBall Kings iliyofanyika katika viunga vya Don Bosco Oysterbay Jijini Dar es Salaam.

"Mchezo ulikuwa mzuri na wenye ushindani mkubwa kwa siku ya jana, makosa yetu tumeyaona ambayo yamepelekea kufungwa kwa 'goal difference 30'. Tunategemea kucheza vizuri zaidi katika mchezo wa pili kwa kuwa tumeshaanza kuyafanyia kazi madhaifu yetu yaliyojitokeza", alisema Msofe. 

Katika hatua nyingine, mashabiki wa timu ya Mchenga BBall Stars wamefurahishwa na kiwango cha timu yao, kilichoonyeshwa siku hiyo hadi kupelekea kuibuka na ushindi mnono katika mechi ya kwanza ya fainali za Sprite BBall Kings kwa mwaka 2017.

Kwa upande mwingine, Mchezo wa fainali ya pili kati ya tano unapigwa Jumatano hii, kwenye viwanja hivyo hivyo vya Don Bosco Oysterbay