Ijumaa , 23rd Jun , 2017

Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi ameishukuru Sportpesa kwa kuileta timu ya Everton ambapo amedai itaweza kusaidia na kubadilisha uzoefu wa kisoka nchini.

Madadi amebainisha hayo wakati akizungumza na wanahabari kwenye ukumbi wa hotel ya Hyatt Regency Jijini Dar es Salaam katika ghafla fupi iliyoandaliwa na uongozi wa Sportpesa Tanzania kuhusu ujio wa timu ya hiyo.

"TFF tunaamini ushirikiano wa SportPesa na Everton utasaidia ukuaji wa soka nchini pamoja na kuendesha kliniki za watoto na vijana juu ya mpira wa miguu. Mimi naona 'program' ya Everton inayo mchango mkubwa wa kutusukuma tusogee haraka haraka, sisi kama Shirikisho tunamuheshimu muwekezaji yeyote anayekuja kutusaidia. Wakijitokeza watu kutupiga jeki kama Sportpesa sisi tunasema Alhamdullilah, tunasema Bwana Yesu asifiwe" alisema Madadi.

Mkurugenzi wa Ufundi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Salum Madadi

Kwa upande wake Mkurugenzi wa utawala na utekelezaji wa Sportpesa Tanzania, Abbas Tarimba amesema ujio wa Everton utasaidia kuitangaza nchi katika ramani ya michezo hususani kuwashawishi maskauti kuja kwa wingi nchini Tanzania kwa ajili ya kutafuta vipaji.

Vile vile Tarimba amesema wamewashawishi klabu ya hiyo katika mchezo wake wa Januari mosi mwakani dhidi ya Manchester United wavae jezi zenye maneno ya kuitangaza Tanzania.

Kwa upande mwingine timu ya Everton inatarajiwa kuingia nchini mnamo Julai 12 ambapo siku hiyo watakuwa na 'training' ya vijana wa (U-15) na baadaye watatoa 'training' UDSM kwa wanafunzi wanaosomea masuala ya michezo. Huku Julai 13 kabla ya mechi watafanya mafunzo kwa timu za vijana wa Simba na Yanga na kumalizia kutoa semina kwa Makocha wa timu hizo na mwishowe kuingia dimbani kuvaana na timu ya Gor Mahia majira kutokea Kenya ya 11 jioni.