Jumanne , 21st Feb , 2017

Timu ya Tenisi ya Walamavu ya Tanzania imefanikiwa kufuzu kushiriki michuano ya Dunia BNP Paribas baada ya kuifunga Kenya kwa Seti 2-0 katika mchezo wa Fainali wa mashindano ya kufuzu ya Afrika yaliyofanyika nchini Kenya.

Timu ya Tennis walemavu wakati ikiagwa Tanzania kuelekea nchi Kenya kwa ajili ya mashindano hayo

Kocha Mkuu wa Timu hiyo Riziki Salum amesema, wamefurahi kuibuka na ushindi na kufanikiwa kuiwakilisha Afrika kwa upande wa wanaume katika michuano ya Dunia.

"Mashindano yalikuwa na ushindani mkubwa kutokana na timu nyingi kujipanga na ukizingatia sisi hatuna maandalizi ya kutosha lakini kujituma kwa wachezaji kumetufanya tuibuke kidedea," amesema.

Salum amesema, kwa upande wa timu ya wanawake imefanikiwa kuibuka na ushindi wa pili baada ya kufungwa na Kenya.

Kocha Riziki Salum

"Nawashukuru wachezaji wangu kwa moyo wao wa kujituma kila tunaposhiriki mashindano makubwa bila kujali hali tunayopitia na naamini tutakaporudi nyumbani tutafanya maandalizi ya kutosha kuelekea michuano ya dunia," amesema.

Kocha Riziki aliwataja wachezaji walioshiriki mashindano hayo kuwa ni Novatus Temba, Juma Hamis, Jumanne Nassor huku kwa upande wa wanawake wakiwa ni Rehema Seleman na Lucy Julius.