Alhamisi , 22nd Jun , 2017

Kikosi cha Taifa Stars kinatarajiwa kuondoka leo jioni nchini kuelekea Afrika Kusini kwa ajili ya kushiriki michuano ya COSAFA itakayotimua vumbi Juni 25 mwaka huu huku wakijiamini kufanya vizuri.

Akiongea na vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam leo, kocha wa Mkuu Salum Mayanga amesema kikosi chake kipo katika hali nzuri kiafya hivyo wanatarajia kufanya vyema katika mashindano hayo.

"Vijana wote wapo sawa tayari kwa michuano ya COSAFA, tunaimani tutafanya vyema. Watanzania watupe sapoti" alisema Mayanga.

Naye Nahodha msaidizi wa kikosi hicho Himid Mao amesema wachezaji wenzake wamejiandaa vizuri katika kutafuta ushindi wa michuano hiyo ili waweze kuendelea mbele katika hatua nyingine.

Taifa Stars imepangwa kundi A ambako wapinzani wake ni Mauritius, Malawi na Angola wakati Kundi B ni Msumbiji, Shelisheli, Madagascar na Zimbabwe. Timu za Botswana, Zambia na Afrika Kusini kadhalika Namibia, Lesotho na Swaziland zitakuwa na mechi maalumu (play off) ili kuingia robo fainali.

Kwa mujibu wa Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga, kikosi kinachoondoka leo ni makipa Aishi Salum Manula  (Azam FC), Benno David Kakolanya  (Young Africans SC) na Said Mohammed Said (Mtibwa Sugar FC).

Walinzi wa pembeni upande wa kulia ni Shomari Salum Kapombe    (Azam FC) na Hassan Hamis Ramadhan 'Kessy' (Young Africans SC) wakati upande wa kushoto wapo Gadiel Michael (Azam FC) na Amim Abdulkarim (Toto Africans FC).

Walinzi wa kati ni Erasto Nyoni  (Azam FC), Salim Hassan Abdallah (Mtibwa Sugar), Abdi Banda (Simba SC) na Nurdin Chona (Tanzania Prisons) wakati viungo wa kuzuia kuwa ni Himid Mao (Azam FC) na Salmin Hoza wa Mbao FC.

Kadhalika wako viungo wa kushambulia ambao ni Mzamiru Yassin Selembe (Simba), Simon Happygod Msuva (Young Africans SC), Raphael Daudi (Mbeya City) na Shizza Ramadhani Kichuya (Simba SC).

Katika safu ya ushambuliaji wamo Thomas Emmanuel Ulimwengu (AFC Eskilstuna – Sweden), Mbaraka Abeid Yusufu (Kagera Sugar), Stamili Mbonde, Elius Maguli (Dhofar SC) na Shabani Idd Chilunda (Azam FC).