Jumatatu , 20th Mar , 2017

Kikosi cha Taifa Stars kimeanza kambi huku wachezaji wengine kutoka kikosi cha Azam FC wakitarajiwa kuingia kambini hii leo usiku huku kikimkosa Mshambuliaji wa Kimataifa Thomas Ulimwengu.

Thomas Ulimwengu

Afisa Habari wa Shirikisho la Soka nchini TFF Alfred Lucas amesema, taarifa ambazo wamezipata kutoka Sweden ni kwamba Ulimwengu kwa sasa yuko chini ya uangalizi wa madaktari wa timu hiyo ya AFC Eskilstuna.

"Kocha alitaja kikosi cha timu ya taifa ambacho kilitakiwa kuingia kambini hapo jana, na wachezaji walioripoti ni kutoka Mtibwa, Ruvu Shooting, Yanga na Simba SC huku wachezaji kutoka katika kikosi cha Azam FC wakiwa bado hawajawasili lakini tunawatarajia kuingia kambini leo usiku," amesema.

"Tumewasiliana na Thomas Ulimwengu na ni majeruhi na anaangaliwa kila siku hivyo tukisema tumlete huku tutaaribu ratiba ya uangalizi wake na kwa msingi huo michezo wa timu ya Taifa ataikosa," amesema.

Hivyo sasa Mayanga atabaki na washambuliaji Mbwana Samatta (KRC Genk- Ubelgiji), Ibrahim Ajib (Simba SC), Mbaraka Yusufu (Kagera Sugar) na Abdul-Rahman Mussa (Ruvu Shooting).

Taifa Stars inatarajiwa kucheza na Botswana Machi 25, 2017 kabla ya kuivaa Burundi Machi 28, mwaka huu katika michezo kirafiki wakati huu wa Kalenda ya Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA).