Ijumaa , 17th Nov , 2017

Ligi kuu ya soka Tanzania bara raundi ya 10 itaendelea wikiendi hii ikianza leo kwa mechi moja ambapo Singida United itakuwa nyumbani kuivaa Lipuli FC.

Singida United inayofundishwa na Hans Van Pluijm ipo katika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi ikiwa na alama 14 wakati Lipuli FC inayofundishwa na Suleiman Matola ikiwa katika nafasi ya saba ikiwa na alama 13. Mshindi wa mechi ya leo atamzidi mwenzake katika msimamo wa ligi.

Wakati huo kesho vinara wa ligi hiyo Simba SC yenye alama 19 itakuwa jijini Mbeya kuivaa Tanzania Prisons yenye alama 14 katika nafasi ya 5. Simba imefanya mazoezi yake ya mwisho leo asubuhi kwenye uwanja wa kumbukumbu ya Sokoine.

Siku ya Jumapili mabingwa watetezi wa ligi hiyo Yanga SC wakiwa na alama 17 katika nafasi ya tatu itashuka kwenye dimba la Uhuru kuivaa Mbeya City yenye alama 11 katika nafasi ya 8.

Mchezo mwingine wa kusisimua utakuwa ni kati ya Azam FC inayoshika nafasi ya pili ikiwa na alama 19 dhidi ya Njombe Mji yenye alama 7 katika nafasi ya 14.