Jumapili , 17th Oct , 2021

Klabu ya wekundu wa msimbazi Simba, wameonyesha kuwa wao ndio wababe wa soka la kimataifa, baada ya jioni ya leo kufanikiwa kuianza safari yao ya matumaini kuelekea kunako nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuichapa Galax Jwaneng huko Botswana bao 2-0.

Nahodha wa Simba, John Bocco akionyesha makali yake dimbani

Mabao ya wanalunyasi, yamesukumiziwa kimiani na kiungo Thaddeo Lwanga dakika ya pili na John Bocco dakika ya 6 ya mchezo.

Simba, inahitaji sare ya aina yoyote katika mchezo wa marudiano utakaochezwa kwenye dimba la Benjamin Mkapa baadae mwezi huu na hata ikipoteza basi kwa tofauti ya bao moja ili itinge hatua ya makundi ya michuano hiyo mikubwa ya vilabu afrika.

Ikumbukwe Simba, ambayo ilicheza bila ya nyota wake Chris Mugalu, Jonas Mkude, Kibu Denis, Yusuph Mhilu na Ousmane Sakho, inawania kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano hiyo baada ya kufika robo fainali mara mbili ndani ya misimu mitatu iliyopita.

Wakati huohuo Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo imewapongeza Simba kwa ushindi wao dhidi ya Galaxy Jwaneng ya Botswana katika mchezo uliochezwa leo huko nchini Botswana.