Jumatano , 18th Jan , 2017

Vinara wa ligi kuu Tanzania Bara imeanza kupoteza mwelekeo wa njia ya ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara baada ya leo kupotea njia kwenye mashamba ya miwa, na kulazimishwa suluhu na wakata miwa wa Mtibwa Sugar

Kiungo wa Mtibwa Ally Shomari akipambana na beki wa Simba Hamad Juma

Katika mchezo huo uliopigwa katika dimba la Jamhuri mjini Morogoro, Simba imeendelea kuonesha 'ubutu' katika safu yake ya ufungaji kwa kutengeneza nafasi nyingi lakini ikishindwa kuzitumia.

Kwa upande wa Mtibwa, waliingia uwanjani wakionesha kukamia mchezo huku wakiwa na mbinu ya kumaliza kwa sare kwa kuweka ukuta imara ulioongozwa na wakongwe Henry Joseph Shindika, Salim Mbonde, Vincent Barnabas, Issa Rashid 'Baba Ubaya' na kiungo Shaaban Nditi, hali iliyopelekea mchezo huo umalizike bila bao kwa upande wowote.

Akizungumzia mchezo huo, Nahodha wa Simba Jonas Mkude amekubali matokeo na kusema mpira una matokeo matatu, hivyo licha ya kutoyapenda, inabidi wayakubali kwa kuwa ndiyo matokeo ya mpira, na kuahidi kufanya vizuri zaidi katika michezo inayofuata.

Mshambuliaji wa Simba Shiza Kichuya baada ya kumfanyia madhambi Rashidi Mandawa  katika mchezo wao wa ligi kuu, Morogoro

Kwa upande wake Nahodha wa Mtibwa Sugar Shaaban Nditi ameshukuru kupata point moja katika mchezo huo, huku akitupia lawama ubovu wa uwanja na kusema wao hawakuzoea kufanya mazoezi katika uwanja huo, hivyo ubovu wa uwanja umechangia kuikosesha timu yake ushindi katika mchezo wa leo.

Matokeo haya yanaifanya Simba iendelee kubaki kileleni kwa kufikisha point 45, ikiwa ni point 2 mbele ya Yanga

Simba na Mtibwa ni timu ambazo wachezaji wake wengi wamewahi kuzichezea timu zote mbili yaani kuna wachezaji wa Simba waliotoka Mtibwa na kuna wachezaji wa Mtibwa waliotoka Simba, hivyo ni timu ambazo wachezaji wake wengi wanafahamiana

Mchezi ya Simba Vs Mtibwa katika mzunguko wa Kwanza ambapo Simba walishinda 2-0 katika uwanja wa Uhuru