Jumanne , 26th Jan , 2021

Wawakilishi wa Tanzania kwenye michuano ya klabu bingwa barani Afrika, 'Wekundu wa Msimbazi', Simba wamethibitisha kumsajili mlinzi wa kati kutoka klabu ya Highlanders na timu ya taifa ya Zimbabwe Peter Muduhwa kandarasi ya mkopo wa miezi sita.

Mlinzi mpya wa Simba, Peter Muduhwa

Muduhwa amesajiliwa na Simba akitokea kwenye majukumu ya timu yake ya taifa ya Zimbabwe  alipokuwa anaiwakilisha nchi yake na kutolewa hatua ya makundi kwenye michuano ya Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa ndani CHAN yanayoendelea nchini Cameroon.

Mlinzi huyo mwenye miaka 27, amesaini kandarasi ya miezi sita yenye kipengele cha makubaliano ya kuongeza mkataba huo endapo Simba wakiridhishwa n akiwango chake na kuonesha nia ya kumbakisha beki huyo kitasa.

Mlinzi huyo mwenye uwezo wa kucheza mlinzi wa kulia ni wazi hautotumika kwenyue michezo ya ligi kuu bara kwasababu dirisha dogo la usajili nchini Tanzania limefungwa lakini atatumika kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika kwa sababu dirisha dogo la usajili la CAF lipo wazi.

Baada ya kufeli majaribio kwenye klabu ya Bidvest Wits ya Afrika Kusini aliyoyafanya na Mzimbabwe mwenzake ambaye hivi sasa ni mshambuliaji wa Azam, Prince Dube pamoja na dili la kwenda kukipiga nchini Sudan, sasa Peter Muduhwa ni mwekundu wa msimbazi.

Usajili wa Peter Muduhwa unakuwa ni usajili wa nne kwa mabingwa hao wa Tanzania bara baada ya kuwasajili Thadeo Lwanga, Perfect Chikwende na Lukosa Junior.