Jumanne , 23rd Mei , 2017

Zikiwa zimepita siku kadhaa tangu klabu ya Yanga kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania bara kwa msimu wa tatu mfululizo, Simba wameamua kuongeza nguvu zao katika fainali ya kombe la shirikisho dhidi ya Mbao FC itakayopigwa Jumamosi Dodoma. 

Mohamed Ibrahim, mchezaji wa Simba SC

Akizungumza mtandao wa Simba mchezaji Mohamed Ibrahim 'Mo Ibrahim' amewataka mashabiki wa Simba kwa kipindi hiki kuongeza nguvu na kutokea kwa wingi siku ya Jumamosi kuwapa nguvu wachezaji ili waweze kushinda mchezo huo na kuchukua kombe hilo kwa kuwa wamekosa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu. 

"Fainali hiyo ya Jumamosi ni muhimu sana kwetu sababu tukishinda tunachukua kombe, mashabiki wajitokeze wengi kuja kushangilia timu yao siyo siri hatutawaangusha sababu kombe kubwa tumelikosa basi hata hili ambalo lipo pembeni itabidi tuchukue, kwa hiyo mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kushangilia ushindi na kombe tunalokwenda kuchukua" alisisitiza 'Mo Ibrahim'

Endapo Simba itatwaa ubingwa huo, itapata nafasi ya kuiwakilisha Tanzania katika michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, fursa ambayo imekosekana Msimazi kwa takriban miaka minne sasa