Ijumaa , 13th Jan , 2017

Klabu ya Azam FC imefanikiwa rasmi kushona midomo ya mashabiki wa watani wa jadi Simba na Yanga baada ya leo kuipiga Simba bao 1-0 katika fainali ya Kombe la Mapinduzi na kutwaa kombe hilo kwa mara tatu.

Kikosi cha Azam kilichotwaa ubingwa

Ushindi huu umekuja ikiwa ni siku chache baada ya kuipiga Yanga mabao 4-0 katika mchezo wa hatua ya makundi, hatua inayofanya utani uliokuwa ukiendelea baina ya mashabiki wa Simba na Yanga kukoma rasmi, kwani timu zote sasa zimechezea kipigo kutoka kwa Azam, tofauti ikiwa ni idadi ya mabao.

Katika mchezo wa leo uliokuwa mgumu na wenye ushindani wa hali ya juu, timu zote mbili zimeonesha kandanda safi kwa kutumia viungo wao, lakini viungo wa Azam walionekana kuwazidia viungo wa Simba na kufanikiwa kupata bao dakika ya 12 ya mchezo kwa shuti kali nje ya 18, lililopigwa na Himid Mao ambaye alifanikiwa kuwahadaa mabeki wa Simba na kumchungulia golikipa ambaye alikuwa mbele kidogo ya goli.

Kipindi cha pili Simba walionesha mchezo mzuri zaidi, na kuongeza mashambulizi, lakini wakini bado tatizo la washambuliaji wake kutokuwa makini katika eneo la kumalizia limeendelea kuonekana kwani washambuliaji wake Juma Luizio, Laudit Mavugo aliyeingia dakika ya 40 na Pastory Athanas aliyeingia dakika za mwisho walishindwa kutumia nafasi kadhaa walizozipata.

Kosakosa zilikuwa pande zote kwani kwa upande wa Azam pia nafasi kadhaa zilishindwa kutumiwa vizuri na kufanya hadi dakika 90 zinakamilika, Azam wakiibuka na ushindi wa bao 1-0, na hivyo Azam kukabidhiwa rasmi kombe la Mapinduzi kwa mwaka huu.

Hadi sasa Azam wamefikisha ubingwa wa 3 sawa na Simba huku ikitoka bila kufungwa goli hata moja.

Golikipa wa Azam FC Aishi Manula (Azam) ameibuka kuwa kipa bora wa mashindano wakati Method Mwanjale (Simba) akiibuka kuwa mchezaji bora wa mashindano na Mfaume Ally akipata zawadi ya mwamuzi bora