Jumanne , 24th Nov , 2020

Kikosi cha mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara, wekundu wa msimbazi Simba kitaondoka nchini kupitia uwanja wa kimataifa wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro kwenda Nigeria kwa ajili ya mchezo wa awali wa ligi ya mabingwa Afrika dhidi ya Plateau United utakaopigwa mwishoni mwa mwezi huu.

Mshambuliaji Chris Mugalu (Kulia) akiwa na kocha msaidizi wa Simba, Seleman Matola(Kushoto) enzi akisaini mkataba wa kuitumikia klabu hiyo yenye maskani yake mitaa ya Msimbazi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika mitandao ya kijamii ya Klabu hiyo imeweka wazi kwamba jumla ya wachezaji 24 wataondoka leo majira ya saa kumi na moja na dakika arobaini na tano jioni wakianzia kutua nchini Ethiopia ambacho kitapumzika hadi siku ya jumatano.

Wawakilishi hao wa nchi wataondoka jijini Addis Ababa siku ya Jumatano asubuhi kwenda Abuja ambako ndiko itacheza dhidi ya Plateau United.

Wachezaji walioondoka ni makipa Aishi Manula, Ally Salum na Beno Kakolanya, walinzi ni Shomari Kapombe, Gadiel Michael, Mohamed Hussein, Erasto Nyoni, Ibrahim Ame, Joash Onyango, Pascal Wawa na Kennedy Juma.

Viungo ni Jonas Mkude, Mzamiru Yassin, Said Ndemla, Rally Bwalya, Hassan Dilunga, Francis Kahata na Clatous Chama.

Washambuliaji ni John Bocco, Medie Kagere, Miraji Athumani, Benard Morrison, Luis Miquissone na Ibrahim Ajibu.

Katika taarifa hiyo ni wazi kwamba mshambuliaji Chris Mugalu hajajumuishwa kikosini kutokana na kuwa majeruhi, huku Charles Ilanfya na mlinzi David Kameta wakisalia nchini.