Jumamosi , 21st Oct , 2017

Ligi kuu ya soka Tanzania bara VPL inaendelea leo kwa jumla ya mechi Sita kupigwa kwenye viwanja tofauti ambapo vinara wa ligi Simba SC watakuwa kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam kuikaribisha Njombe Mji.

Simba ambayo ina alama 12 baada ya raundi Sita leo itaingia uwanjani saa 10:00 jioni kusaka alama zingine tatu kwenye raundi ya Saba ya VPL kisha baada ya hapo itajiandaa na raundi ya Nane ambayo itakuwa dhidi ya Yanga Oktoba 28.

Simba inaingia kwenye mchezo wa leo ikiwa na mabadiliko kwenye benchi lake la ufundi ambapo kocha mpya msaidizi Masoud Juma atasimama kwenye mstari baada ya kuchukua nafasi ya Jackson Mayanja aliyejiuzulu mapema wiki hii.

Taarifa kutoka Simba zimeeleza kuwa baada ya mchezo wa leo timu itasafiri kwenda Visiwani Zanzibar kwaajili ya Kambi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya watani wao wa Jadi Yanga ambao kesho watakuwa mkoani Shinyanga kucheza na Stand United.

Mechi za leo

Mbao FC vs Azam FC, Lipuli FC vs Majimaji FC,

Mbeya City vs Ruvu Shooting, Ndanda FC vs Singida United

Mtibwa Sugar vs Tanzania Prisons.