Ijumaa , 13th Jan , 2017

Klabu ya Real Madrid imeweka rekodi mpya katika soka la Hispania kwa kucheza michezo 40 bila kupoteza baada ya kulazimisha sare ya 3-3 dhidi ya Sevilla katika mchezo wa Kombe la Mfalme uliopigwa usiku wa kuamkia leo.

Real Madrid wakishangilia bao la Asensio

 Sare hiyo ilipatikana kwa bao la Karim Benzema la dakika ya 93 na kuipiku Barcelona yenye rekodi ya kucheza mechi 39 bila kupoteza.

Mabao mengine ya Real Madrid yalifungwa na Sergio Ramos na Asensio na kuifanya ifuzu hatua ya robo fainali kwa jumla ya mabao 6-3.

Kipigo cha mwisho kwa timu hiyo chini ya Kocha Mkuu Zinedine Zidane kilikuja Aprili mwaka jana wakati timu hiyo ilipopoteza mechi ya kwanza ya Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya dhidi ya Wolfsburg ya Ujerumani na tangu wakati huo, haijafungwa mechi hata moja katika mashindano yote.

Barcelona ndio klabu ambayo walikuwa na rekodi ya zamani ya kucheza michezo 39 bila kupoteza mechi hata moja na timu hiyo, maarufu kama The Catalans, waliweka rekodi hiyo chini ya meneja Luis Enrique kati ya 2015 na 2016.