Jumanne , 15th Aug , 2017

Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage ameitaka timu ya Mabingwa wa ligi kuu Tanzania Bara Yanga, wajiandae kupokea kichapo kitakatifu katika mechi ya Ngao ya Jamii itakayochezwa mnamo Agosti 23 mwaka huu katika uwanja wa Taifa.

Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba, Ismail Aden Rage.

Aden Rage amefunguka hayo ikiwa zimebaki siku chache kuanza kwa mtifuano huo huku akiwashangaa wanayanga kwa uwamuzi waliyoufanya kuenda kujificha mjini Pemba.

"Kama mimi ningekuwa kiongozi wa Yanga tarehe 23, ningesema hiyo Ngao ya Jamii wazee chukueni maana kila nikiangalia pale wa kumzuia Emmanuel Okwi, John Boko sioni, sasa Haruna Niyonzima naye zile majaro anazozitupa zinaleta raha, kwa hiyo nina uhakika tarehe Agosti  23, al manusura kama wamepata bahati watakula 7, sasa wanakuja kukutana na Simba. Sisi huko nyuma hatujapata ubingwa muda mrefu ni sawa sawa na Simba aliyejeruhiwa ukikukuta naye njiani hana msalie Mtume lazima akumalize tu. Na sijui wameenda Pemba kufanya nini, labda wanaenda tu kuchuma karafuu,” alisema Ismail Rage

Pamoja na hayo, timu ya Simba na Yanga zote kwa pamoja zimekimbilia mjini Zanzibar kwa lengo la kujiweka sawa kuelekea mtanange huo wa kukata na shoka ambao mpaka sasa kila mmoja anamtambia mwenzake kumfunga kutokana na ubora wa usajili waliyofanya katika msimu mpya wa Ligi kuu Tanzania Bara 2017/2018.