Jumapili , 23rd Jul , 2017

Taifa Stars imetolewa katika mashindano ya kusaka tiketi ya kucheza fainali zijazo za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) baada ya kutoka suluhu na Rwanda (Amavubi) katika mchezo uliopigwa jana kwenye Uwanja wa Nyamirambo jijini Kigali.

Amavubi imefanikiwa kusonga mbele kwa faida ya bao la ugenini walilopata katika mechi ya kwanza iliyopigwa Jumamosi iliyopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambayo timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1, wageni Amavubi wakitangulia kufunga huku nahodha wa Stars Himid Mao akisawazisha kwa njia ya penalti.

Katika mchezo huo Taifa Stars wanatakiwa kujilaumu zaidi kutokana na kushindwa kutumia vema nafasi mbalimbali za kufunga walizotengeneza baada ya mabeki wa Amavubi kushindwa kwenda na kasi yao.

Baadhi ya nafasi hizo ni ile ya dakika ya tisa kupitia kwa mshambuliaji John Bocco kupiga shuti lililoishia kupanguliwa na kipa wa Amavubi Eric Ndayishimiye.

Dakika ya 41 pia Stars ilipoteza nafasi ya kufunga kupitia kwa Simon Msuva ambaye shuti lake lilidakwa.