Jumanne , 28th Jun , 2022

Mshambuliaji wa zamani wa klabu Liverpool Divock Origi yuko nchini Italia tayari kwa ajili ya kufanya vipomo vya afya kabla ya kujiunga rasmi na klabu ya AC Milan kwa uhamisho huru.

Divock Origi

Hapo awali Ilitangazwa kuwa Origi ataondoka Liverpool mara tu mkataba wake utakapo malizika mwishoni mwa msimu uliokwisha.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 alifunga mabao muhimu kwa klabu hiyo yenye maskani yake kwenye viunga vya  Anfield, ikiwa ni pamoja na katika ushindi wao wa 2-0 dhidi ya Tottenham katika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 2019.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ubelgiji alijiunga na Liverpool msimu wa mwaka 2014 na kufanikiwa kufunga mabao 41 katika michezo 175 aliyocheza klabuni hapo.

Klabu ya AC Milan wamekuwa mabingwa wa ligi kuu ya Italia serie A kwa mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja uliopita, baada ya kuwazidi wapinzani wao Inter Milan kwa tofauti ya alama mbili.