Jumapili , 25th Jun , 2017

Makamu wa Rais wa zamani wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Athumani Nyamlani amejitoa kwenye kinyang'anyiro cha kuwania urais wa shirikisho hilo unaotarajiwa kufanyika Agosti 12, mwaka huu.

Athumani Nyamlani (kushoto) siku aliyochukua fomu ya urais TFF

Nyamlani aliwasilisha barua TFF leo Jumapili Juni 25, mwaka huu ikiwa ni siku moja tu tangu Kamati ya Uchaguzi ipitishe jina lake kuwa miongoni mwa wagombea 10 wanaowania nafasi hiyo ya urais,sababu aliyoeleza ni masuala binafsi.

Kwa msingi huo, wagombea wanaobaki kwenye kinyang'anyiro na kuhitajika kufika kwenye usaili kuanzia Juni 29, mwaka huu ni tisa wakiongozwa na Rais wa sasa, Jamal Malinzi anayetetea nafasi.

Mbali ya Malinzi wengine wanaowania nafasi hiyo ni Imani Madega, Wallace Karia, Fredrick Masolwa, Fredrick Mwakalebela, John Kijumbe, Shija Richard, Ally Mayay na Emmanuel Kimbe.