Jumamosi , 27th Mei , 2017

Simba SC ya Dar es Salaam na Mbao FC ya Mwanza leo zinakutana Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma kwenye fainali za kuwania Kombe la Shirikisho l katika mchezo utakaoanza saa 10.00 jioni.

Tayari timu zote ziko mjini Dodoma na zimekuwa zikirushiana tambo za hapa na pale, wakati Simba wakiwa wamekamia kutwaa kombe hilo ili kujihakikishia ushiriki katika miachuano ya Kimataifa ambayo imeikosa kwa miaka takriban mitano.

Kwa upande wa Mbao, wao wanataka kuweka historia mpya katika soka la Tanzania kuwa timu ya kwanza kupanda daraja kwa 'Mlango wa Nyuma' na kisha kufuzu michuano ya Kimataifa.

Mbao FC pia inawania kuwa timu ya pili ya Mwanza kupata tiketi ya kucheza michuano ya Afrika, baada ya Pamba SC kufanya hivyo miaka ya nyuma.

Mchezo wa leo unatarajiwa kuchezeshwa na Ahmed Kikumbo wa Dodoma, atakayesaidiwa na Mohammed Mkono wa Tanga na Omary Juma wa Dodoma wakati mwamuzi wa akiba ni Florence Zablon pia wa Dodoma na Kamisaa ni Peter Temu wa Arusha.

Mshindi wa mchezo wa fainali (Kwa msimu huu kati ya Simba na Mbao), ndiye akayekuwa Bingwa wa Kombe la ASFC - HD, atapewa Kombe la Ubingwa na zawadi ya fedha kiasi cha shilingi milioni hamisini (50,000,000/-) kama zilivyoainishwa kwenye waraka wa zawadi wa michuano.

Mara ya mwisho timu hizo zilipokutana Aprili 10, mwaka huu Simba ilitoka nyuma kwa mabao 2-0 na kushinda 3-2 ndani ya dakika 10 za mwisho katika mchezo wa Ligi Kuu Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza hiyo ilifanya Simba iwe imeifunga Mbao katika mechi zote za msimu, mechi zote zilizozikutanisha timu hizo kihistoria, baada ya Oktoba 20, mwaka jana kushinda pia 1-0 katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Uwanja wa Taifa.