Ijumaa , 15th Sep , 2017

Ndanda FC imetamba kuondoka na alama 6 kwenye michezo yake miwili ya ligi kuu Tanzania bara mkoani Mbeya ambapo tayari imeshachukua alama 3 dhidi ya wenyeji Mbeya City wiki iliyopita na kesho inakutana na Prisons.

Msemaji wa Ndanda FC, Idris Bandali amesema kuwa timu yao imejiandaa vyema kwa wiki nzima ikiwa Mbeya na wanasubiri kuchukua alama tatu mbele ya wenyeji Prisons kwenye mchezo wa raundi ya tatu ligi kuu Tanzania Bara.

"Timu imejiandaa vyema, wiki yote hii tumekuwa hapa Mbeya wachezaji wamezoea hali ya hewa na tunategemea tutacheza vizuri na kuondoka na alama 3 ili kutimiza sita katika mechi zetu za Mbeya", amesema Bandali.

Bandalli pia ameeleza kuwa ripoti ya mwalimu baada ya mazoezi ya leo asubuhi inaonesha hakuna majeruhi yoyote kwenye timu hivyo wachezaji wote wapo tayarI kwa mchezo wa kesho. Ndanda ina alama 3 ikiwa imeshinda mechi moja na kupoteza moja dhidi ya Azam FC.