Jumanne , 26th Sep , 2017

Mashindano ya kuogelea ya kanda ya tatu ya Afrika (Cana zone 3) yamepangwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 19 -21 ambapo nchi mbalimbali zimezidi kuthibitisha ushiriki wao.

Rwanda na Sudani zimethibitisha kushiriki michuano hiyo zikiungana na nchi nyingine sita zilizothibitisha kwa mujibu wa mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Chama Cha kuogelea nchini (TSA), Leena Kapadia.

Kapadia amezitaja nchi hizo kuwa ni Afrika Kusini, Zambia, Kenya, Uganda, Djibouti na wenyeji Tanzania huku zaidi ya waogeleaji 200 wanatarajiwa kushiriki katika mashindano hayo ambayo Tanzania ni mabingwa watetezi.

Kapadia amesema kuwa bado wametoa nafasi kwa nchi nyingine kuthibitisha kushiriki hadi wiki moja kabla ya mashindano ili kuleta mvuto na ushindani zaidi.

Nchi ambazo zimeongezewa muda wa kuthibitisha ni Ethiopia, Eritrea, Somalia, Sudani Kusini ambazi zipo kanda ya tatu na za kanda ya nne ni Angola, Botswana, Comoro, Madagascar, Lesotho, Malawi, Mauritius, Seychelles, Msumbiji, Namibia, Zimbabwe na Swaziland.