Jumatatu , 13th Feb , 2017

Beki kisiki wa kati tegemeo wa Simba, Mzimbabwe Method Mwanjali yuko hatarini kuukosa mchezo dhidi ya mahasimu wa jadi, Yanga Februari 25, mwaka huu.

Beki kisiki wa kati wa Simba Method Mwanjali akitibiwa.

Miamba hiyo ya soka nchini, Simba na Yanga itavaana katika mechi ya Mzunguko wa Pili wa Ligi Kuu ya soka Tanzania Bara Jumamosi ya Februari 25 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwanjali anaweza kuukosa mchezo huo baada ya kuumia katika mechi nyingine ya Ligi Kuu dhidi ya Prisons ya Mbeya, Simba wakishinda 3-0 katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mwanjali aliye katika msimu wake wa kwanza Simba SC, alitolewa kwa machela na nafasi yake kuchukuliwa na kiungo Mwinyi Kazimoto katika dakika ya 62.

Meneja wa Simba SC, Mussa Hassan Mgosi amesema kwamba kuna muda mrefu kabla ya mechi na Yanga na hatarajii maumivu ya Mwanjali yatakuwa makali kiasi cha kumuweka nje Februari 25.

“Naona muda bado upo sana, tena wa kutosha. Sitarajii kama atakuwa ameumia kwa kiasi kikubwa,” alisema Mgosi.

Taarifa zaid kutoka klabuni humo zinadai kuwa daktari wa timu amesema huenda Mwanjali akaanza mazoezi mepesi wiki ijayo, lakini haina uhakika kwa asilimia kubwa kama ataweza kuwa fiti hadi Februari 25.