Ijumaa , 18th Aug , 2017

Mwamuzi maarufu katika mchezo wa kandanda nchini Somalia amepigwa risasi na kuuawa karibu na nyumbani kwake mjini Mogadishu wakati akirejea nyumbani kwake mtaa wa Wardhigley akitokea msikitini.

Taarifa zinasema kuwa mwamuzi huyo Osman Jama Dirah, ambaye alisimamia mechi za kanda na kimataifa ameuawa na wanaume wawili waliomfyatulia risasi kadhaa pasipo kugundulika chanzo cha watu hao kufanya hivyo. 

Mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Somalia Anas Ali Mohamud amenukuliwa akisema aliwaona washambuliaji wakiondoka eneo la mauaji na baadaye maafisa wa usalama walifika eneo hilo  lakini kufikia hawajafanikiwa kuwakamata wahusika.

Kwa mujibu wa mwandishi wa BBC Somali Ahmed Adan anasema kuuawa kwa Osman Jama Dirah ni pigo kubwa kwa tasnia ya soka nchini Somalia pamoja na sekta yote ya michezo nchini humo.

Osman Dirah alikuwa miongoni mwa marefa maarufu zaidi nchini humo tangu kusambaratika kwa serikali kuu miaka 27 iliyopita na alifahamika kama mwamuzi bora zaidi na alihudumu katika kamati ya waamuzi katika Shirikisho la Soka la Somalia.

Dirah alianza kushiriki katika kandanda mwaka 1979, kama mlinda lango wa timu ya Galgadud, na baadaye akajiunga na timu ya taifa kama mlinda lango huku mwaka 1997 akiteuliwa kuwa mwamuzi na FIFA nchini Somalia.