Jumapili , 19th Nov , 2017

Mtibwa Sugar imejinasibu kuwa itamfunga kocha wake wa zamani Mecky Mexime ambaye anaifundisha klabu ya Kagera Sugar kwenye mchezo wa ligi kuu leo jioni.

Msemaji wa klabu hiyo Thobias Kifaru amesema kuwa undugu watauweka kando na kucheza soka ambalo litawapa matokeo mbele ya Kagera Sugar ambayo inafundishwa na mchezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar.

“Ni kweli Mexime amecheza kwenye klabu yetu kwa miaka 12 na baadae akawa kocha mkuu wa kikosi chetu lakini leo tutweka pembeni undugu kwasababu tunataka pointi tatu ili tuendeleze rekodi yetu ya kutofungwa msimu huu”, amesema Kifaru.

Mtibwa na Kagera zinakutana katika mchezo wa raundi ya 10 kwenye uwanja wa Manungu huku historia ikiandikwa ambapo wachezaji wa zamani wa Mtibwa Sugar Mecky Mexime na Shabaan Katwila wakiziongoza timu hizo.

Mtibwa Sugar ipo nafasi ya 4 ikiwa na alama 17, wakati Kagera Sugar ipo katika nafasi ya 14 ikiwa na alama 7. Mtibwa haijapoteza mechi hadi sasa na imetoka sare moja tu kwenye uwanja wake wa nyumbani dhidi ya Singida United.