Jumapili , 15th Jan , 2017

Mwanariadha wa Tanzania Alphonce Felix Simbu aliyeibuka mshindi na kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya riadha ya dunia ya Mumbai Marathoni yaliyofanyika nchini India, amefichua siri ya ushindi wake

Alphonce Felix akimalizia mbio zake za Mumbai Marathon

Simbu ametumia masaa 2 dakika 9 na sekunde 32, na kuwapiku Joshua Kirkorir wa Kenya aliyetumia saa 2, dakika 9 na sekunde 50 na Eliud Barbgetuny pia wa Kenya alishika nafasi ya tatu kwa kutumia saa 2 dakika 10 na sekunde 39.

Akizungumzia ushindi huo, Simbu amesema siri kubwa ya ushindi wake katika mbio hizo ni mazoezi aliyoyafanya katika milima mbalimbali ya Tanzania, yaliyomfanya awe imara zaidi katika mazingira ya mashindano hayo yalikuwa yanakabiliwa na kona pamoja na vilima vingi

Jambo lingine lililomsaidia ni uzoefu alioupata katika mashindano mengine ikiwemo Olimpiki za mwaka jana na mashindano ya ubingwa wa dunia ya Beijing mwaka 2015.

Alphonce Felix Simbu (Katikati) 

Kwa ushindi huo, Simbu anatia kibindoni kiasi cha dola za Marekani 67,000 zaidi ya shilingi milioni 140 za kitanzania.

Simbu anakumbukwa pia kwa kuipeperusha bendera ya Tanzania vyema katika mashindano ya Olimpiki yaliyofanyika nchini India mwaka jana kwa kukamata nafasi ya tano katika mbio za marathoni.

Katika mashindano hayo, Mkenya Bornes Kitur amefanikiwa kushinda mbio hizo kwa upande wa wanawake.