Jumapili , 19th Mar , 2017

Bao pekee la mshambuliaji Laudit Mavugo raia wa Burundi limetosha kuivusha Simba SC hadi hatua ya nusu fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho, baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Madini SC.

Laudit Mavugo katika moja ya mechi zake

Katika mechi hiyo ya robo fainali iliyopigwa katika dimba la Sheikh Amri Abeid Arusha, Simba licha ya kushusha 'full muziki' katika kikosi chake, imekutana na ushindani mkali kutoka kwa vijana hao wa Madini inayoshiriki ligi daraja la pili, kiasi cha kumaliza dakika 45 za kipindi cha kwanza bila bao kwa kila upande.

Safu ya ushambuliaji ya Simba iliyoongozwa na Ibrahim Ajib na Laudit Mavugo iliyosaidiwa kwa ukaribu na Shiza Kichuya na Mohamed Ibrahim ilishindwa kutumia nafasi kadhaa ilizopata licha ya kukosekana kwa pasi makini za mwisho, huku vijana wa Madini pia wakiwa hawana uoga wowote na kuonesha uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kuifanya mashambulizi.

Ilikuwa ni dakika ya 54 ya mchezo ambapo Mavugo alitumia udhaifu wa beki wa Madini aliyeshindwa ku-'control' mpira wa juu uliomfikia akiwa kama beki wa mwisho, na Mavugo kumzidi uwezo na kuunganisha kwa kichwa kilichompita golikipa wa madini aliyekuwa mbali kidogo na goli.

Juuko Murshid

Katika mechi ya leo safu ya ulinzi ya Simba imeongozwa na Mganda Juuko Murshid ambaye hajaonekana kikosini tangu mwaka jana kutokana na matatizo aliyokutana nayo ikiwemo msiba pamoja na kushiriki michuano ya AFCON.

Murshid mwenyewe anasema anaamini kuwa uwezo wake unamruhusu kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza, hivyo atajitahidi kumshawishi mwalimu kwa njia ya mazoezi na bidii awapo uwanjani

Kwa matokeo hayo, Simba inaungana na Mbao FC ya Mwanza katika hatua ya nusu fainali, huku timu nyingine mbili zikisubiriwa.