Alhamisi , 22nd Jun , 2017

Katibu Mkuu wa Klabu ya Mabingwa wa Ligii kuu Tanzania Bara Young Africans, Charles Boniface Mkwasa amelaani vikali kitendo cha mashabiki wa timu yake kuchoma moto jezi ya aliyekuwa mchezaji wao kwa kusema kitendo hicho kinashusha heshima ya timu.

Katibu Mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwasa

Mkwasa amebainisha hayo masaa machache yaliyopita tokea mashabiki na wapenzi wa klabu hiyo kuchukizwa na kitendo cha kuondoka kwa Nahodha Haruna Niyonzima, na kupelekea kuchoma moto jezi yenye namba nane mgongoni ambayo ndiyo aliyokuwa anavaa kipindi akiingia uwanjani.

"Wanachama niwaombe wawe na utulivu wawe na umakini haya mambo ni ya kawaida katika mchezo na Haruna kutoka kwenda timu nyingine siyo mara ya kwanza kwa wachezaji waliowahi kupitia Yanga, wapo wengi wamepitia lakini hakikuwa kitendo kama hicho kwa hiyo mimi nakikemea sikiungi mkono na ninawaombe wale wengine waliyokuwa na mawazo kama hayo wasiwe na mawazo hayo wajaribu kuwa na umoja huu. Mpira ni ushindani na kujenga uhusiano mzuri" alisema Mkwasa.

Pamoja na hayo, Mkwasa amesema kitendo hicho kinawadhalilisha wao wenyewe mashabiki wanaofanya hivyo pamoja na klabu nzima kwa ujumla kwa kudai jezi hiyo ina nembo inayotambulisha timu yao.